Maktaba yote ya Kiislamu

76 - The Man - Al-'Insān

:1

Hakika kilimpitia binaadamu kipindi katika zama ambacho kwamba hakuwa kitu kinacho tajwa.

:2

Hakika Sisi tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyo changanyika, tumfanyie mtihani. Kwa hivyo tukamfanya mwenye kusikia, mwenye kuona.

:3

Hakika Sisi tumembainishia Njia. Ama ni mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru.

:4

Hakika Sisi tumewaandalia makafiri minyororo na pingu na Moto mkali.

:5

Hakika watu wema watakunywa katika vinywaji vilivyo changanyika na kafuri,

:6

Ni chemchem watakao inywa waja wa Mwenyezi Mungu, wakiifanya imiminike kwa wingi.

:7

Wanatimiza ahadi, na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea sana,

:8

Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa.

:9

Hakika sisi tunakulisheni kwa wajihi wa Mwenyezi Mungu. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani.

:10

Hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu Mlezi hiyo siku yenye shida na taabu.

:11

Basi Mwenyezi Mungu atawalinda na shari ya siku hiyo, na atawakutanisha na raha na furaha.

:12

Na atawajazi Bustani za Peponi na maguo ya hariri kwa vile walivyo subiri.

:13

Humo wataegemea juu ya viti vya enzi, hawataona humo jua kali wala baridi kali.

:14

Na vivuli vyake vitakuwa karibu yao, na mashada ya matunda yataning'inia mpaka chini.

:15

Na watapitishiwa vyombo vya fedha na vikombe vya vigae,

:16

Vya fedha safi kama kiyoo, wamevipima kwa vipimo.

:17

Na humo watanyweshwa kinywaji kilicho changanyika na tangawizi.

:18

Hiyo ni chemchem iliyo humo inaitwa Salsabil.

:19

Na watawazungukia kuwatumikia wavulana wasio pevuka, ukiwaona utawafikiri ni lulu zilizo tawanywa.

:20

Na utakapo yaona, utakuwa umeona neema na ufalme mkubwa.

:21

Juu yao zipo nguo za hariri laini za kijani kibichi, na hariri nzito ya at'ilasi. Na watavikwa vikuku vya fedha, na Mola wao Mlezi atawanywesha kinywaji safi kabisa.

:22

Hakika haya ni malipo yenu; na juhudi zenu zimekubaliwa.

:23

Hakika Sisi tumekuteremshia Qur'ani kidogo kidogo.

:24

Basi ngojea hukumu ya Mola wako Mlezi wala usimt'ii miongoni mwao mwenye dhambi au mwenye kufuru.

:25

Na likumbuke jina la Mola wako Mlezi asubuhi na jioni;

:26

Na usiku msujudie Yeye, na umtakase usiku, wakati mrefu.

:27

Kwa hakika watu hawa wanapenda maisha ya kidunia, na wanaiacha nyuma yao siku nzito.

:28

Sisi tumewaumba, na tukavitia nguvu viungo vyao. Na tukitaka tutawabadilisha mfano wao wawe badala yao.

:29

Hakika haya ni mawaidha; basi anaye taka atashika Njia ya kwenda kwa Mola wake Mlezi.

:30

Wala hamwezi kutaka ila atakapo Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye ilimu, Mwenye hikima.

:31

Humuingiza amtakaye katika rehema yake. Na wenye kudhulumu amewawekea adhabu iliyo chungu.