Maktaba yote ya Kiislamu

44 - The Smoke - Ad-Dukhān

:1

H'a Mim

:2

Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha,

:3

Hakika tumekiteremsha katika usiku ulio barikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji.

:4

Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima,

:5

Jambo litokalo kwetu. Hakika Sisi ndio wenye kutuma.

:6

Ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.

:7

Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, ikiwa nyinyi mna yakini.

:8

Hakuna mungu ila Yeye; anahuisha na anafisha- Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa mwanzo.

:9

Lakini wao wanacheza katika shaka.

:10

Basi ingoje siku ambayo mbingu zitakapo leta moshi ulio dhaahiri,

:11

Utakao wafunika watu: Hii ni adhabu chungu!

:12

Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu hii. Hakika tutaamini.

:13

Nini faida ya kukumbuka kwao? Na alikwisha wafikia Mtume mwenye kubainisha.

:14

Na wao wakamgeuzia uso, na wakasema: Huyu amefunzwa, naye ni mwendawazimu.

:15

Hakika sisi tutaiondoa adhabu kidogo, lakini nyinyi kwa yakini mtarejea vile vile!

:16

Siku tutayo yashambulia mashambulio makubwa, bila ya shaka Sisi ni wenye kutesa.

:17

Na hakika kabla ya hawa tuliwafanyia mtihani watu wa Firauni, na aliwafikia Mtume Mtukufu.

:18

Akasema: Nipeni waja wa Mwenyezi Mungu; kwa hakika mimi kwenu ni Mtume Muaminifu.

:19

Na msimfanyie kiburi Mwenyezi Mungu; hakika mimi nitakuleteeni uthibitisho ulio wazi.

:20

Nami najikinga kwa Mola wangu Mlezi na ndiye Mola wenu Mlezi pia, ili msinipige mawe.

:21

Na ikiwa hamniamini, basi jitengeni nami.

:22

Ndipo akamwomba Mola wake Mlezi: Hakika watu hawa ni wakosefu.

:23

Mwenyezi Mungu akasema: Basi nenda na waja wangu usiku. Kwa yakini mtafuatwa.

:24

Na iache bahari vivyo hivyo imeachana, hakika wao hao ni jeshi litakalo zamishwa.

:25

Mabustani mangapi, na chemchem ngapi waliziacha!

:26

Na mimea na vyeo vitukufu!

:27

Na neema walizo kuwa wakijistareheshea!

:28

Ndio hivyo! Na tukawarithisha haya watu wenginewe.

:29

La mbingu wala ardhi hazikuwalilia, wala hawakupewa muhula.

:30

Na bila ya shaka tuliwaokoa Wana wa Israili katika adhabu ya kuwadhalilisha,

:31

Ya Firauni. Hakika yeye alikuwa jeuri katika wenye kupindukia mipaka.

:32

Na tuliwakhiari kwa ujuzi wetu kuliko walimwengu wenginewe.

:33

Na tukawapa katika ishara zenye majaribio yaliyo wazi.

:34

Hakika hawa wanasema:

:35

Hapana ila kufa kwetu mara ya kwanza tu, wala sisi hatufufuliwi.

:36

Basi warudisheni baba zetu, ikiwa nyinyi mnasema kweli.

:37

Je! Ni wao bora au watu wa Tubbaa' na walio kuwa kabla yao? Tuliwaangamiza. Hakika hao walikuwa wakosefu.

:38

Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake kwa mchezo.

:39

Hatukuviumba hivyo ila kwa Haki, lakini wengi wao hawajui.

:40

Hakika siku ya Uamuzi ni wakati ulio wekwa kwa wao wote.

:41

Siku ambayo rafiki hatamfaa rafiki yake kwa chochote, wala hawatanusuriwa.

:42

Isipo kuwa atakaye mrehemu Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

:43

Hakika Mti wa Zaqqum,

:44

Ni chakula cha mwenye dhambi.

:45

Kama shaba iliyo yayushwa, hutokota matumboni

:46

Kama kutokota kwa maji ya moto.

:47

(Itasemwa:) Mkamateni na mtupeni katikati ya Jahannamu!

:48

Kisha mmwagieni juu ya kichwa chake adhabu ya maji yanayo chemka.

:49

Onja! Ati wewe ndiye mwenye nguvu, mtukufu!

:50

Hakika haya ndiyo mliyo kuwa mkiyatilia shaka.

:51

Hakika wachamngu watakuwa katika mahali pa amani,

:52

Katika mabustani na chemchem,

:53

Watavaa hariri nyepesi na hariri nzito wakikabiliana,

:54

Hivi ndivyo itakavyo kuwa, na tutawaoza mahurilaini.

:55

Humo watataka kila aina ya matunda, na wakae kwa amani.

:56

Humo hawataonja mauti ila mauti yale ya kwanza, na (Mwenyezi Mungu) atawalinda na adhabu ya Jahannamu,

:57

Kuwa ni fadhila zitokazo kwa Mola wako Mlezi. Huko ndiko kufuzu kukubwa.

:58

Basi tumeifanya nyepesi hii Qur'ani kwa ulimi wako, ili wapate kukumbuka.

:59

Ngoja tu, na wao wangoje pia.