Maktaba yote ya Kiislamu

43 - The Ornaments of Gold - Az-Zukhruf

:1

H'a Mim

:2

Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha.

:3

Hakika Sisi tumeifanya Qur'ani kwa Kiarabu ili mfahamu.

:4

Na hakika hiyo imo katika Asili ya Maandiko yalioko kwetu, ni tukufu na yenye hikima.

:5

Je! Tuache kukukumbusheni kabisa kwa kuwa nyinyi ni watu mlio pita mipaka kwa ukafiri?

:6

Na Manabii wangapi tuliwatuma kwa watu wa zamani!

:7

Na hawajii Nabii yeyote ila walikuwa wakimkejeli.

:8

Na tuliwaangamiza walio kuwa na nguvu kushinda wao. Na mfano wa watu wa zamani umekwisha pita.

:9

Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Kaziumba Mwenye nguvu, Mjuzi,

:10

Ambaye amekufanyieni ardhi kama tandiko, na akakufanyieni ndani yake njia mpate kuongoka.

:11

Na ambaye ndiye aliye teremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi, na kwa hayo tukaifufua nchi iliyo kufa. Na namna hivi ndivyo mtakavyo tolewa.

:12

Na ambaye ndiye aliye umba katika kila kitu jike na dume, na akakufanyieni marikebu na wanyama mnao wapanda.

:13

Ili mkae vizuri migongoni mwao, kisha mkumbuke neema za Mola wenu Mlezi mnapokaa sawa sawa juu yao na mseme: Ametakasika aliye mfanya huyu atutumikie, na tusingeli weza kufanya haya wenyewe.

:14

Na hakika sisi tutarudi kwa Mola wetu Mlezi.

:15

Na wanamfanyia katika waja wake fungu. Kwa hakika mwanaadamu ni mtovu wa fadhila aliye dhaahiri.

:16

Au amejichukulia watoto wanawake katika vile alivyo viumba, na akakuteulieni nyinyi watoto wanaume?

:17

Na anapo bashiriwa mmoja wao kwa yale aliyo mpigia mfano Mwenyezi Mungu, uso wake husawijika na hujaa hasira.

:18

Ati aliye lelewa katika mapambo, na katika mabishano hawezi kusema kwa bayana...?

:19

Na wakawafanya Malaika, ambao ni waja wa Mwingi wa Rehema, ni wanawake! Kwani wameshuhudia kuumbwa kwao? Ushahidi wao utaandikwa na wao watahojiwa!

:20

Nao husema: Angeli penda Mwingi wa Rehema tusingeli waabudu sisi. Hawana ujuzi wowote wa hayo! Hawana ila kusema uwongo tu!

:21

Kwani tuliwapa Kitabu kabla ya hichi, na ikawa wao wanakishikilia hicho?

:22

Bali wanasema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, basi na sisi tunaongoza nyayo zao.

:23

Na kadhaalika hatukumtuma mwonyaji kwenye mji wowote ila watu wake walio deka kwa starehe walisema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, na sisi tunafuata nyayo zao.

:24

Akasema (Mwonyaji): Hata nikikuleteeni yenye uwongofu bora kuliko mlio wakuta nao baba zenu? Wakasema: Sisi tunayakataa tu hayo mliyo tumwa.

:25

Basi tukawalipizia. Angalia ulikuwaje mwisho wa walio kadhibisha!

:26

Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Hakika mimi ninajitenga mbali na hayo mnayo yaabudu,

:27

Isipo kuwa yule aliye niumba, kwani Yeye ataniongoa.

:28

Na akalifanya hili liwe neno lenye kubaki katika vizazi vyake ili warejee.

:29

Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka ikawafikia Haki na Mtume aliye bainisha.

:30

Na ilipo wafikia Haki wakasema: Huu ni uchawi, na sisi hakika tunaukataa.

:31

Na walisema: Kwa nini Qur'ani hii haikuteremshwa kwa mtu mkubwa katika miji miwili hii?

:32

Kwani wao ndio wanao gawa rehema za Mola wako Mlezi? Sisi tumewagawanyia baina yao maisha yao katika uhai wa duniani, na tukawanyanyua baadhi yao juu ya wengine kwa daraja nyingi; kwa hivyo baadhi yao wanawafanya wenginewe wawatumikie. Na rehema za Mwenyezi Mungu ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya.

:33

Na lau isinge kuwa watu watakuwa kundi moja tungeli wajaalia wanao mkufuru Rahmani wana nyumba zao zina dari ya fedha, na ngazi zao pia wanazo pandia,

:34

Na milango ya nyumba zao na vitanda wanavyo egemea juu yake,

:35

Na mapambo. Lakini hayo si chochote ila ni starehe ya maisha ya dunia tu, na Akhera iliyoko kwa Mola wako Mlezi ni ya wenye kumchamngu.

:36

Anaye yafanyia upofu maneno ya Rahmani tunamwekea Shet'ani kuwa ndiye rafiki yake.

:37

Na hakika wao wanawazuilia Njia na wenyewe wanadhani kuwa wameongoka.

:38

Hata atakapo tujia atasema: Laiti ungeli kuwako baina yangu na wewe kama umbali baina ya mashariki na magharibi. Rafiki mwovu mno wewe!

:39

Na kwa kuwa mlidhulumu, haitakufaeni kitu leo kwamba nyinyi mnashirikiana katika adhabu.

:40

Je! Unaweza kuwasikilizisha viziwi, au unaweza kuwaongoa vipofu na waliomo katika upotofu ulio wazi?

:41

Na hata tukikuondoa, Sisi tutalipiza kisasi chetu kwao.

:42

Au tutakuonyesha tulio waahidi. Nasi bila ya shaka tuna uweza juu yao.

:43

Basi wewe yashike yaliyo funuliwa kwako. Hakika wewe uko kwenye Njia Iliyo Nyooka.

:44

Na hakika haya ni ukumbusho kwako na kwa kaumu yako. Na mtakuja ulizwa.

:45

Na waulize Mitume wetu tulio watuma kabla yako: Je! Tulifanya miungu mingine iabudiwe badala ya Rah'mani?

:46

Na bila ya shaka tulimtuma Musa kwa Ishara zetu ende kwa Firauni na waheshimiwa wake, na akasema: Hakika mimi ni Mtume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote!

:47

Lakini alipo wajia na Ishara zetu wakaingia kuzicheka.

:48

Na hatukuwaonyesha Ishara yoyote ila hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuliko nyenginewe. Na tukawakamata kwa adhabu ili warejee.

:49

Na wakasema: Ewe mchawi! Tuombee kwa Mola wako Mlezi kwa ile ahadi aliyo kuahidi; hakika sisi tutakuwa wenye kuongoka.

:50

Basi tulipo waondolea adhabu hiyo, mara wakaingia kuvunja ahadi.

:51

Na Firauni alitangaza kwa watu wake, akisema: Enyi watu wangu! Kwani mimi sinao huu ufalme wa Misri, na hii mito inapita chini yangu? Je! Hamwoni?

:52

Au mimi si bora kuliko huyu aliye mnyonge, wala hawezi kusema waziwazi?

:53

Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu, au hawakuja Malaika pamoja naye wakamwandama?

:54

Basi aliwachezea watu wake, na wakamt'ii. Kwa hakika hao walikuwa watu wapotovu.

:55

Walipo tukasirisha tuliwapatiliza tukawazamisha wote!

:56

Kisha tukawafanya kuwa watangulizi na mfano kwa wa baadaye.

:57

Na alipo pigiwa mfano Mwana wa Mariamu, watu wako waliupiga ukelele.

:58

Wakasema: Miungu yetu kwani si bora kuliko huyu? Hawakukupigia mfano huo ila kwa ubishi tu. Bali hao ni watu wagomvi!

:59

Hakuwa yeye (Isa) ila ni Mtumwa tuliye mneemesha na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili.

:60

Na tungeli penda tungeli wafanyia miongoni mwenu Malaika katika ardhi wakifuatana.

:61

Na kwa hakika yeye ni alama ya Saa ya Kiyama. Basi usiitilie shaka, na nifuateni. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.

:62

Wala asikuzuilieni Shet'ani. Hakika yeye ni adui yenu wa dhaahiri.

:63

Na alipo kuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: Nimekujieni na hikima, na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyo khitalifiana. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnit'ii mimi.

:64

Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na ni Mola wenu Mlezi. Basi Muabuduni Yeye tu. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.

:65

Lakini makundi kwa makundi yao yalikhitalifiana wao kwa wao. Ole wao walio dhulumu kwa adhabu ya siku chungu.

:66

Je! Nini wanangojea ila Saa iwajie kwa ghafla na wala wao hawatambui?

:67

Siku hiyo marafiki watakuwa ni maadui, wao kwa wao, isipo kuwa wachamngu.

:68

Enyi waja wangu! Hamtakuwa na khofu siku hiyo, wala hamtahuzunika.

:69

Ambao waliziamini Ishara zangu na walikuwa Waislamu.

:70

Ingieni Peponi, nyinyi na wake zenu; mtafurahishwa humo.

:71

Watakuwa wanapitishiwa sahani za dhahabu na vikombe; na vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia, na nyinyi mtakaa humo milele.

:72

Na hiyo ni Pepo mliyo rithishwa kwa hayo mliyo kuwa mkiyafanya.

:73

Mnayo humo matunda mengi mtakayo yala.

:74

Kwa hakika wakosefu watakaa katika adhabu ya Jahannamu.

:75

Hawatapumzishwa nayo na humo watakata tamaa.

:76

Wala Sisi hatukuwadhulumu, bali wao ndio walio kuwa madhaalimu.

:77

Nao watapiga kelele waseme: Ewe Malik! Na atufishe Mola wako Mlezi! Naye aseme: Hakika nyinyi mtakaa humo humo!

:78

Kwa yakini tulikuleteeni Haki, lakini wengi katika nyinyi mlikuwa mnaichukia Haki.

:79

Au waliweza kupitisha amri yao? Bali ni Sisi ndio tunao pitisha.

:80

Au wanadhani kwamba hatusikii siri zao na minong'ono yao? Wapi! Na wajumbe wetu wapo karibu nao, wanayaandika.

:81

Sema: Ingeli kuwa Rahmani ana mwana, basi mimi ningeli kuwa wa kwanza kumuabudu.

:82

Ametakasika Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, Mola Mlezi wa A'rshi, na hayo wanayo msifia.

:83

Basi waache wapige porojo wakicheza mpaka wakutwe na hiyo siku yao waliyo ahidiwa.

:84

Na Yeye ndiye Mungu mbinguni, na ndiye Mungu katika ardhi. Naye ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi.

:85

Na ametukuka Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo ndani yake. Na uko kwake ujuzi wa Saa ya Kiyama, na kwake Yeye mtarudishwa.

:86

Wala hao mnao waomba badala yake Yeye hawana uweza wa kumwombea mtu, isipo kuwa anaye shuhudia kwa haki, na wao wanajua.

:87

Na ukiwauliza ni nani aliye waumba? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu! Basi ni wapi wanako geuziwa?

:88

Na usemi wake (Mtume) ni: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hawa ni watu wasio amini.

:89

Basi wasamehe, na uwambie maneno ya salama. Watakuja jua.