Maktaba yote ya Kiislamu

36 - Ya Sin - Yā-Sīn

:1

Ya-Sin (Y. S.).

:2

Kwa Haki ya Qur'ani yenye hikima!

:3

Hakika wewe ni miongoni mwa walio tumwa,

:4

Juu ya Njia Iliyo Nyooka.

:5

Uteremsho wa Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

:6

Ili uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa, basi wao wamekuwa wenye kughafilika.

:7

Bila ya shaka kauli imekwisha thibiti juu ya wengi katika wao, kwa hivyo hawaamini.

:8

Tumeweka makongwa shingoni mwao, yakawafika videvuni. Kwa hivyo vichwa vyao viko juu tu.

:9

Tumeweka kizuizi mbele yao, na kizuizi nyuma yao, na tumewafunika macho yao; kwa hivyo hawaoni.

:10

Ni sawa sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawataamini.

:11

Hakika wewe unamwonya mwenye kufuata ukumbusho, na akamcha Arrahman, Mwingi wa Rehema, kwa ghaibu. Basi mbashirie huyo msamaha na ujira mwema.

:12

Hakika Sisi tunawafufua wafu, na tunayaandika wanayo yatanguliza, na wanayo yaacha nyuma. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari asli lenye kubainisha.

:13

Na wapigie mfano wa wakaazi wa mji walipo wafikia walio tumwa.

:14

Tulipo watumia wawili, wakawakanusha. Basi tukawazidishia nguvu kwa mwingine wa tatu. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwenu.

:15

Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi. Na Mwingi wa Rehema hakuteremsha kitu. Nyinyi mnasema uwongo tu.

:16

Wakasema: Mola wetu Mlezi anajua kwamba hakika sisi tumetumwa kwenu.

:17

Wala si juu yetu ila kufikisha ujumbe ulio wazi.

:18

Wakasema: Sisi tumeagua kuwa nyinyi ni wakorofi. Ikiwa hamtaacha basi kwa yakini tutakupigeni mawe, na mtapata adhabu chungu kutoka kwetu.

:19

Wakasema: Ukorofi wenu mnao wenyewe! Je! Ni kwa kuwa mnakumbushwa? Ama nyinyi ni watu walio pindukia mipaka.

:20

Na akaja mtu mbio kutokea upande wa mbali wa mjini, akasema: Enyi watu wangu! Wafuateni hawa walio tumwa.

:21

Wafuateni ambao hawakutakini ujira, hali ya kuwa wenyewe wameongoka.

:22

NA KWA NINI nisimuabudu yule aliye niumba na kwake mtarejeshwa?

:23

Je! Niishike miungu mingine badala yake? Arrahmani, Mwingi wa Rehema, akinitakia madhara uombezi wa hao hautanifaa kitu, wala hawataniokoa.

:24

Basi hakika mimi hapo nitakuwa katika upotovu ulio dhaahiri.

:25

Hakika mimi nimemuamini Mola wenu Mlezi, basi nisikilizeni!

:26

Akaambiwa: Ingia Peponi! Akasema: Laiti kuwa watu wangu wangeli jua

:27

Jinsi Mola wangu Mlezi alivyo nisamehe, na akanifanya miongoni mwa walio hishimiwa.

:28

Na hatukuwateremshia kaumu yake baada yake jeshi kutoka mbinguni, wala si wenye kuteremsha.

:29

Hakukuwa ila ukelele mmoja tu; na mara walizimwa!

:30

Nawasikitikia waja wangu. Hawajii Mtume ila wao humkejeli.

:31

Je! Hawaoni umma ngapi tulizo ziangamiza kabla yao? Hakika hao hawarejei tena kwao.

:32

Na hapana mmoja ila wote watakusanywa waletwe mbele yetu.

:33

Na Ishara hiyo kwao - ardhi iliyo kufa, nasi tukaifufua, na tukatoa ndani yake nafaka, wakawa wanazila!

:34

Na tukafanya ndani yake mabustani ya mitende na mizabibu, na tukatimbua chemchem ndani yake,

:35

Ili wale matunda yake, na hayo hayakufanywa na mikono yao! Basi je, hawashukuru?

:36

Subhana, Ametakasika, aliye umba dume na jike vyote katika vinavyo mea katika ardhi na katika nafsi zao, na katika wasivyo vijua.

:37

Na usiku ni Ishara kwao. Tunauvua humo mchana, mara wao wanakuwa gizani.

:38

Na jua linakwenda kwa kiwango chake. Hayo ni makadirio ya Mwenye nguvu, Mwenye kujua.

:39

Na mwezi tumeupimia vituo, mpaka unakuwa kama karara kongwe.

:40

Haliwi jua kuufikia mwezi, wala usiku kuupita mchana. Na vyote vinaogelea katika njia zao.

:41

Na ni Ishara kwao kwamba Sisi tuliwapakia dhuriya zao katika jahazi ilio sheheni.

:42

Na tukawaumbia kutoka mfano wake wanavyo vipanda.

:43

Na tukitaka tunawazamisha, wala hapana wa kuwasaidia, wala hawaokolewi,

:44

Isipo kuwa kwa rehema zitokazo kwetu na starehe kwa muda.

:45

Na wanapo ambiwa: Jilindeni na yalioko mbele yenu na yalioko nyuma yenu, ili mpate kurehemewa...

:46

Na haiwafikii Ishara yoyote katika Ishara za Mola wao Mlezi ila wao huwa ni wenye kuipuuza.

:47

Na wanapo ambiwa: Toeni katika aliyo kupeni Mwenyezi Mungu, walio kufuru huwaambia walio amini: Je! Tuwalishe ambao Mwenyezi Mungu angependa angeli walisha mwenyewe? Nyinyi hammo ila katika upotofu ulio dhaahiri.

:48

Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi ni wakweli?

:49

Hawangojei ila ukelele mmoja tu utakao wachukua nao wamo kuzozana.

:50

Basi hawataweza kuusia, wala kwa watu wao hawarejei.

:51

Na litapulizwa barugumu, mara watatoka makaburini wakikimbilia kwa Mola wao Mlezi.

:52

Watasema: Ole wetu! Nani aliye tufufua kwenye malazi yetu? Haya ndiyo aliyo yaahidi Mwingi wa Rehema na wakasema kweli Mitume.

:53

Haitakuwa ila ukelele mmoja tu, mara wote watahudhuruishwa mbele yetu.

:54

Basi leo nafsi yoyote haitadhulumiwa kitu, wala hamtalipwa ila yale mliyo kuwa mkiyatenda.

:55

Hakika watu wa Peponi leo wamo shughulini, wamefurahi.

:56

Wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya fakhari.

:57

Watapata humo kila namna ya matunda na watapata kila watakacho kitaka.

:58

"Salama!" Hiyo ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mlezi Mwenye kurehemu.

:59

Na enyi wakosefu! Jitengeni leo!

:60

Je! Sikuagana nanyi, enyi wanaadamu, kuwa msimuabudu Shet'ani? Hakika yeye ni adui dhaahiri kwenu.

:61

Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.

:62

Na bila ya shaka yeye amekwisha lipoteza kundi kubwa miongoni mwenu. Je, hamkuwa mkifikiri?

:63

Hii basi ndiyo Jahannamu mliyo kuwa mkiahidiwa.

:64

Ingieni leo kwa vile mlivyo kuwa mkikufuru.

:65

Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyachuma.

:66

Na tungeli penda tungeli yafutilia mbali macho yao, wakawa wanaiwania njia. Lakini wange ionaje?

:67

Na tungeli taka tunge wageuza sura hapo hapo walipo, basi wasinge weza kwenda wala kurudi.

:68

Na tunaye mzeesha tunamrudisha nyuma katika umbo. Basi je! hawazingatii?

:69

Wala hatukumfundisha (Muhammad) mashairi, wala hayatakikani kwake hayo. Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur'ani inayo bainisha.

:70

Ili imwonye aliye hai, na neno litimie juu ya makafiri.

:71

Je! Hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyo fanya mikono yetu wanyama wa mifugo, na wao wakawa wenye kuwamiliki.

:72

Na Sisi tukawadhalilishia. Basi baadhi yao wako wanao wapanda, na baadhi yao wanawala.

:73

Na wao wanapata kwao manufaa na vinywaji. Basi je, hawashukuru?

:74

Na wameishika miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu ili ati wapate kusaidiwa!

:75

Hawataweza kuwasaidia. Bali hao ndio watakuwa askari wao watakao hudhurishwa.

:76

Basi maneno yao yasikuhuzunishe. Hakika Sisi tunayajua wanayo yaweka siri na wanayo yatangaza.

:77

Kwani mwanaadamu haoni ya kwamba Sisi tumemuumba yeye kutokana na tone la manii? Kisha sasa yeye ndio amekuwa ndiye mgomvi wa dhaahiri!

:78

Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake, akasema: Ni nani huyo atakaye ihuisha mifupa nayo imekwisha mung'unyika?

:79

Sema: Ataihuisha huyo huyo aliye iumba hapo mara ya mwanzo. Na Yeye ni Mjuzi wa kila kuumba.

:80

Aliye kujaalieni kupata moto kutokana na mti wa kijani nanyi mkawa kwa huo mnawasha.

:81

Kwani aliye ziumba mbingu na ardhi hawezi kuwaumba mfano wao? Kwani! Naye ndiye Muumbaji Mkuu, Mjuzi.

:82

Hakika amri yake anapo taka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa.

:83

Basi Ametakasika yule ambaye mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu; na kwake Yeye mtarejeshwa.