Maktaba yote ya Kiislamu

72 - The Jinn - Al-Jinn

:1

Sema: Imefunuliwa kwangu ya kuwa kundi moja la majini lilisikiliza, na likasema: Hakika sisi tumeisikia Qur'ani ya ajabu!

:2

Inaongoza kwenye uwongofu, kwa hivyo tumeiamini, wala hatutamshirikisha yeyote na Mola wetu Mlezi.

:3

Na kwa hakika utukufu wa Mola wetu Mlezi umetukuka kabisa; hana mke wala mwana.

:4

Na kwa hakika wapumbavu miongoni mwetu walikuwa wakisema uwongo ulio pindukia mipaka juu ya Mwenyezi Mungu.

:5

Nasi tulidhani kuwa watu na majini hawamzulii uwongo Mwenyezi Mungu.

:6

Na hakika walikuwako wanaume katika watu walio kuwa wakitafuta kujikinga kwa wanaume wa kijini; kwa hivyo wakawazidisha madhambi.

:7

Na kwa hakika wao walidhani, kama mlivyo dhani nyinyi, ya kuwa Mwenyezi Mungu hatamleta Mtume.

:8

Nasi tulizigusa mbingu, na tukaziona zimejaa walinzi wenye nguvu na vimondo.

:9

Na hakika tulikuwa tukikaa humo katika baadhi ya makao ili kusikiliza; lakini sasa anaye taka kusikiliza atakuta kimondo kinamvizia!

:10

Nasi hatujui kama wanatakiwa shari wale wanao kaa kwenye ardhi au Mola wao Mlezi anawatakia uwongofu.

:11

Na hakika katika sisi wamo walio wema, na wengine wetu ni kinyume na hivyo. Tumekuwa njia mbali mbali.

:12

Nasi tulijua kuwa hatutomshinda Mwenyezi Mungu duniani, wala hatuwezi kumponyoka kwa kukimbia.

:13

Nasi tulipo usikia uwongofu tuliuamini. Basi mwenye kumuamini Mola wake Mlezi basi haogopi kupunjwa wala kudhulumiwa.

:14

Na hakika wamo katika sisi Waislamu, na wamo kati yetu wanao acha haki. Basi walio silimu, hao ndio walio tafuta uwongofu.

:15

Na ama wanao acha haki, hao watakuwa kuni za Jahannamu.

:16

Na lau kama wangeli simama sawasawa juu ya njia tungeli wanywesha maji kwa wingi,

:17

Ili tuwajaribu kwa hayo. Na anaye puuza kumkumbuka Mola wake Mlezi atamsukuma kwenye adhabu ngumu.

:18

Na hakika misikiti ni ya Mwenyezi Mungu, basi msimuabudu yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu.

:19

Na hakika Mja wa Mwenyezi Mungu alipo simama kumwomba, wao walikuwa karibu kumzonga!

:20

Sema: Hakika mimi namwomba Mola wangu Mlezi, wala simshirikishi Yeye na yeyote.

:21

Sema: Mimi sina mamlaka ya kukudhuruni wala kukuongozeni.

:22

Sema: Hakika hapana yeyote awezae kunilinda na Mwenyezi Mungu, wala sitapata pa kukimbilia isipo kuwa kwake Yeye tu.

:23

Ila nifikishe Ujumbe utokao kwa Mwenyezi Mungu na risala zake. Na wenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika hao watapata Moto wa Jahannamu wadumu humo milele.

:24

Hata watakapo yaona wanayo ahidiwa, ndipo watakapo jua ni nani mwenye msaidizi dhaifu, na mchache wa idadi.

:25

Sema: Sijui kama yapo karibu hayo mnayo ahidiwa, au Mola wangu Mlezi atayawekea muda mrefu.

:26

Yeye ndiye Mwenye kujua ya siri, wala hamdhihirishii yeyote siri yake,

:27

Isipo kuwa Mtume wake aliye mridhia. Naye huyo humwekea walinzi mbele yake na nyuma yake.

:28

Ili Yeye ajue kwamba wao wamefikisha ujumbe wa Mola wao Mlezi, na Yeye anayajua vyema yote walio nayo, na amedhibiti idadi ya kila kitu.