Maktaba yote ya Kiislamu
1

T'aa Siin Miim. (T'. S. M.)

2

Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha.

3

Huenda labda ukajikera nafsi yako kwa kuwa hawawi Waumini.

4

Tunge penda tungeli wateremshia kutoka mbinguni Ishara zikanyenyekea shingo zao.

5

Wala hauwafikii ukumbusho mpya kutoka kwa Arrahman ila wao hujitenga nao.

6

Kwa yakini wamekanusha; kwa hivyo zitakuja wafikia khabari za yale waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha.

7

Je! Hawakuiona ardhi, mimea mingapi tumeiotesha humo, ya kila namna nzuri?

8

Hakika katika haya zipo Ishara. Lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

9

Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

10

Na Mola wako Mlezi, alipo mwita Musa, akamwambia: Fika kwa watu madhaalimu,

11

Watu wa Firauni. Hawaogopi?

12

Akasema: Hakika mimi nachelea wasinikanushe.

13

Na kifua changu kina dhiki, na ulimi wangu haukunjuki vyema. Basi mtumie ujumbe Harun.

14

Na wao wana kisasi juu yangu, kwa hivyo naogopa wasije kuniuwa.

15

Akasema: Siyo hivyo kabisa! Nendeni na miujiza yetu. Hakika Sisi tu pamoja nanyi, tunasikiliza.

16

Basi mfikieni Firauni na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

17

Waachilie Wana wa Israili wende nasi.

18

(Firauni) akasema: Sisi hatukukulea wewe utotoni, na ukakaa kwetu katika umri wako miaka mingi?

19

Na ukatenda kitendo chako ulicho tenda, nawe ukawa miongoni mwa wasio na shukrani?

20

(Musa) akasema: Nilitenda hayo hapo nilipo kuwa miongoni mwa wale walio potea.

21

Basi nikakukimbieni nilipo kuogopeni, tena Mola wangu Mlezi akanitunukia hukumu, na akanijaalia niwe miongoni mwa Mitume.

22

Na hiyo ndiyo neema ya kunisumbulia, na wewe umewatia utumwani Wana wa Israili?

23

Firauni akasema: Na nani huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote?

24

Akasema: Ndiye Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi ni wenye yakini.

25

(Firauni) akawaambia walio mzunguka: Hamsikilizi?

26

(Musa) akasema: Ndiye Mola wenu Mlezi, na Mola Mlezi wa baba zenu wa kwanza.

27

(Firauni) akasema: Hakika huyu Mtume wenu aliye tumwa kwenu ni mwendawazimu.

28

(Musa) akasema: Ndiye Mola Mlezi wa Mashariki na Magharibi na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi mnatia akilini.

29

(Firauni) akasema: Ukimfuata mungu mwengine asiye kuwa mimi, basi bila ya shaka nitakufunga gerezani.

30

Akasema: Je! Ijapo kuwa nitakuletea kitu cha kubainisha wazi?

31

Akasema: Kilete basi, kama wewe ni katika wasemao kweli.

32

Basi akaitupa fimbo yake, mara ikawa nyoka wa kuonekana dhaahiri.

33

Na akautoa mkono wake, na mara ukawa mweupe kwa watazamao.

34

(Firauni) akawaambia waheshimiwa walio mzunguka: Hakika huyu ni mchawi mtaalamu.

35

Anataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake. Basi mna shauri gani?

36

Wakasema: Mpe muda yeye na nduguye na uwatume mijini wapigao mbiu ya mgambo.

37

Wakuletee kila mchawi bingwa mtaalamu.

38

Basi wakakusanywa wachawi wakati na siku maalumu.

39

Na watu wakaambiwa: Je! Mtakusanyika?

40

Huenda tutawafuata wachawi wakiwa wao ndio watakao shinda.

41

Basi walipo kuja wachawi wakamwambia Firauni: Je! Tutapata ujira tukiwa sisi ndio tulio shinda?

42

Naam! Na hakika mtakuwa katika watu wa mbele.

43

Musa akwaambia: Tupeni mnavyo taka kutupa.

44

Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na wakasema: Kwa nguvu za Firauni hakika sisi hapana shaka ni wenye kushinda.

45

Musa tena akatupa fimbo yake, nayo mara ikavimeza walivyo vizua.

46

Hapo wachawi walipinduka wakasujudu.

47

Wakasema: Tunamuamini Mola Mlezi wa walimwengu wote.

48

Mola Mlezi wa Musa na Harun.

49

(Firauni) akasema: Je! Mmemuamini kabla sijakuruhusuni? Bila ya shaka yeye basi ndiye mkubwa wenu aliye kufunzeni uchawi. Basi mtakuja jua! Nitakata mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakubandikeni misalabani nyote.

50

Wakasema: Haidhuru, kwani sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi.

51

Hakika sisi tunatumai Mola wetu Mlezi atatusamehe makosa yetu, kwa kuwa ndio wa kwanza wa kuamini.

52

Na tulimuamrisha Musa kwa wahyi: Nenda na waja wangu wakati wa usiku. Kwa hakika mtafuatwa.

53

Basi Firauni akawatuma mijini wapiga mbiu za mgambo.

54

(Wakieneza): Hakika hawa ni kikundi kidogo.

55

Nao wanatuudhi.

56

Na sisi ni wengi, wenye kuchukua hadhari.

57

Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem,

58

Na makhazina, na vyeo vya hishima,

59

Kadhaalika; na tukawarithisha hayo Wana wa Israili.

60

Basi wakawafuata lilipo chomoza jua.

61

Na yalipo onana majeshi mawili haya, watu wa Musa wakasema: Hakika sisi bila ya shaka tumepatikana!

62

(Musa) akasema: Hasha! Hakika yu pamoja nami Mola wangu Mlezi. Yeye ataniongoa!

63

Tulimletea wahyi Musa tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana, na kila sehemu ikawa kama mlima mkubwa.

64

Na tukawajongeza hapo wale wengine.

65

Tukawaokoa Musa na walio kuwa pamoja naye wote.

66

Kisha tukawazamisha hao wengine.

67

Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara; lakini wengi wao si katika wenye kuamini.

68

Na kwa hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

69

Na wasomee khabari za Ibrahim.

70

Alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini?

71

Wakasema: Tunaabudu masanamu, daima tunayanyenyekea.

72

Akasema: Je! Yanakusikieni mnapo yaita?

73

Au yanakufaeni, au yanakudhuruni?

74

Wakasema: Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo hivyo.

75

Je! Mmewaona hawa mnao waabudu-

76

Nyinyi na baba zenu wa zamani?

77

Kwani hakika hao ni adui zangu, isipo kuwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

78

Ambaye ndiye aliye niumba, na Yeye ndiye ananiongoa,

79

Na ambaye ndiye ananilisha na kuninywesha.

80

Na ninapo ugua ni Yeye ndiye anaye niponesha.

81

Na ambaye atanifisha, na kisha atanihuisha.

82

Na ambaye ndiye ninaye mtumai kunisamehe makosa yangu Siku ya Malipo.

83

Mola wangu Mlezi! Nitunukie hukumu na uniunganishe na watendao mema.

84

Na unijaalie nitajwe kwa wema na watu watakao kuja baadaye.

85

Na unijaalie katika warithi wa Bustani za neema.

86

Na umsamehe baba yangu, kwani hakika alikuwa miongoni mwa wapotovu.

87

Wala usinihizi Siku watapo fufuliwa.

88

Siku ambayo kwamba mali hayato faa kitu wala wana.

89

Isipo kuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi.

90

Na Pepo itasogezwa kwa wachamngu.

91

Na Jahannamu itadhihirishwa kwa wapotovu.

92

Na wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwaabudu

93

Badala ya Mwenyezi Mungu? Je! Wanakusaidieni, au wanajisaidia wenyewe?

94

Basi watavurumizwa humo wao na hao wakosefu,

95

Na majeshi ya Ibilisi yote.

96

Watasema, na hali ya kuwa wanazozana humo:

97

Wallahi! Kwa yakini tulikuwa katika upotovu ulio dhaahiri,

98

Tulipo kufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote.

99

Na hawakutupoteza ila wale wakosefu.

100

Basi hatuna waombezi.

101

Wala rafiki wa dhati.

102

Laiti tungeli pata kurejea tena tungeli kuwa katika Waumini.

103

Hakika katika haya ipo Ishara, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

104

Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

105

Kaumu ya Nuhu waliwakadhibisha Mitume.

106

Alipo waambia ndugu yao, Nuhu: Je! Hamchimngu?

107

Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.

108

Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.

109

Na sikutakini juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

110

Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.

111

Wakasema: Je! Tukuamini wewe, hali wanao kufuata ni watu wa chini?

112

Akasema: Nayajuaje waliyo kuwa wakiyafanya?

113

Hisabu yao haiko ila kwa Mola wao Mlezi, laiti mngeli tambua!

114

Wala mimi si wa kuwafukuza Waumini.

115

Mimi si cho chote ila ni Mwonyaji wa dhaahiri shaahiri.

116

Wakasema: Ikiwa huachi, ewe Nuhu, bila ya shaka utapigwa mawe.

117

Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikanusha.

118

Basi hukumu baina yangu na wao kwa hukumu yako, na uniokoe mimi na walio pamoja nami, Waumini.

119

Kwa hivyo tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye katika marikebu iliyo sheheni.

120

Kisha tukawazamisha baadaye walio bakia.

121

Hakika katika haya ipo Ishara, lakini si wengi wao walio kuwa Waumini.

122

Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

123

Kina A'd waliwakanusha Mitume.

124

Alipo waambia ndugu yao, Hud: Je! Hamchimngu?

125

Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.

126

Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.

127

Wala sikutakeni juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

128

Je! Mnajenga juu ya kila mnyanyuko kumbusho la kufanyia upuuzi?

129

Na mnajenga majengo ya fakhari kama kwamba mtaishi milele!

130

Na mnapo tumia nguvu mnatumia nguvu kwa ujabari.

131

Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini.

132

Na mcheni aliye kupeni haya mnayo yajua.

133

Amekupeni wanyama wa kufuga na wana.

134

Na mabustani na chemchem.

135

Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku Kubwa.

136

Wakasema: Ni mamoja kwetu, ukitupa mawaidha au hukuwa miongoni mwa watoao mawaidha.

137

Haya si chochote ila ni mtindo wa watu wa tokea zamani.

138

Wala sisi hatutaadhibiwa.

139

Wakamkanusha; nasi tukawaangamiza. Hakika bila ya shaka katika haya ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.

140

Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

141

Kina Thamud waliwakanusha Mitume.

142

Alipo waambia ndugu yao Saleh: Je! Hamumchimngu?

143

Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.

144

Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini.

145

Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

146

Je! Mtaachwa salama usalimina katika haya yaliyopo hapa?

147

Katika mabustani, na chemchem?

148

Na konde na mitende yenye makole yaliyo wiva.

149

Na mnachonga milimani majumba kwa ustadi.

150

Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.

151

Wala msit'ii amri za walio pindukia mipaka,

152

Ambao wanafanya ufisadi katika nchi, wala hawatengenezi.

153

Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa walio rogwa.

154

Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi. Basi lete Ishara ukiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.

155

Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa, na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalumu.

156

Wala msimguse kwa uwovu, isije ikakushikeni adhabu ya Siku Kubwa.

157

Lakini wakamuuwa, na wakawa wenye kujuta.

158

Basi ikawapata adhabu. Hakika katika hayo ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.

159

Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

160

Watu wa Lut'i waliwakanusha Mitume.

161

Alipo waambia ndugu yao, Lut'i: Je! Hamumchimngu?

162

Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu kwenu.

163

Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nit'iini mimi.

164

Wala mimi sikutakini ujira juu yake; ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

165

Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume?

166

Na mnaacha alicho kuumbieni Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Ama kweli nyinyi ni watu mnao ruka mipaka!

167

Wakasema: Ewe Lut'i! Usipo acha, hapana shaka utakuwa miongoni mwa wanao tolewa mji!

168

Akasema: Hakika mimi ni katika wanao kichukia hichi kitendo chenu.

169

Mola wangu Mlezi! Niokoe mimi na ahali zangu na haya wayatendayo.

170

Basi tukamwokoa yeye na ahali zake wote,

171

Isipo kuwa kikongwe katika walio kaa nyuma.

172

Kisha tukawaangamiza wale wengine.

173

Na tukawanyeshea mvua, basi ni ovu mno mvua ya waliyo onywa.

174

Hakika katika hayo ipo Ishara. Na hawakuwa wengi wao wenye kuamini.

175

Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

176

Watu wa Machakani waliwakanusha Mitume.

177

Shuaibu alipo waambia: Je! Hamfanyi mkamchamngu?

178

Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.

179

Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.

180

Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

181

Timizeni kipimo sawa sawa, wala msiwe katika wanao punja.

182

Na pimeni kwa haki iliyo nyooka;

183

Wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye jeuri kwa ufisadi.

184

Na mcheni aliye kuumbeni nyinyi na vizazi vilivyo tangulia.

185

Wakasema: Hakika wewe ni katika walio rogwa.

186

Na wewe si chochote ila ni mtu tu kama sisi, na kwa yakini tunakuona wewe ni katika waongo.

187

Hebu tuangushie vipande kutoka mbinguni ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.

188

Akasema: Mola wangu Mlezi anajua zaidi mnayo yatenda.

189

Basi walimkanusha, na ikawashika adhabu ya siku ya kivuli. Hakika hiyo ilikuwa adhabu ya siku kubwa.

190

Hakika katika hayo ipo Ishara, lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.

191

Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

192

Na bila ya shaka hii ni Uteremsho wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

193

Ameuteremsha Roho muaminifu,

194

Juu ya moyo wako, ili uwe katika Waonyaji,

195

Kwa ulimi wa Kiarabu ulio wazi.

196

Na hakika bila ya shaka haya yamo katika Vitabu vya kale.

197

Je! Haikuwa kwao ni Ishara kwamba wanayajua haya wanazuoni wa Wana wa Israili?

198

Na lau kuwa tungeli iteremsha juu ya mmoja wa wasio kuwa Waarabu,

199

Na akawasomea, wasingeli kuwa wenye kuamini.

200

Namna hivi tunaingiza katika nyoyo za wakosefu.

201

Hawataiamini mpaka waione adhabu chungu.

202

Basi itawafikia kwa ghafla, na hali hawana khabari.

203

Na watasema: Je, tutapewa muhula?

204

Basi, je, wanaihimiza adhabu yetu?

205

Waonaje kama tukiwastarehesha kwa miaka,

206

Kisha yakawafikia waliyo kuwa wakiahidiwa,

207

Yatawafaa nini yale waliyo stareheshewa?

208

Wala hatukuangamiza mji wo wote ila ulikuwa na waonyaji -

209

Kuwa ni ukumbusho. Wala Sisi hatukuwa wenye kudhulumu.

210

Wala Mashet'ani hawakuteremka nayo,

211

Wala haitakiwi kwao, na wala hawawezi.

212

Hakika hao wametengwa na kusikia.

213

Basi usimwombe mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa watakao adhibiwa.

214

Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe.

215

Na watwae kwa upole wanao kufuata miongoni mwa Waumini.

216

Na ikiwa watakuasi basi sema: Mimi najitenga mbali na hayo mnayo yatenda.

217

Na umtegemee Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

218

Ambaye anakuona unapo simama,

219

Na mageuko yako kati ya wanao sujudu.

220

Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua.

221

Je! Nikwambieni nani wanawashukia Mashet'ani?

222

Wanamshukia kila mzushi mkubwa mwingi wa dhambi.

223

Wanawapelekea yale wanayo yasikia; na wengi wao ni waongo.

224

Na watungaji mashairi ni wapotofu ndio wanawafuata.

225

Je! Huwaoni kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde?

226

Na kwamba wao husema wasiyo yatenda?

227

Isipo kuwa wale walio amini, na wakatenda mema, na wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi, na wakajitetea wanapo dhulumiwa. Na wanao dhulumu watakuja jua mgeuko gani watakao geuka.